Maafisa wa kikosi cha Polisi wa Kenya wakionea fahari bendera ya taifa lao baada ya kutua nchini Haiti katika juhudi za kurejesha amani nchini humo. Picha|Reuters
ILI kuonyesha ushirikiano wake na juhudi zake katika kuleta amani nchini Haiti, Serikali sasa imeanza ‘kuuza’ utamaduni wa Kenya kwa ulimwengu.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya polisi wa Kenya waliotumwa nchini humo kupata ushindi baada ya kukomboa mji wa Gauthier.
Katibu katika Wizara ya Mambo ya nje, Dkt Korir Sing’oei amesema kuwa Kenya itaendelea kusaidia Haiti ili kuhakikisha kuwa amani inapatikana katika taifa hilo.
“Kenya itaendelea kuisaidia Haiti hadi amani itakapopatikana. Tunatazamia Haiti iliyo imara na itakayostawi kwa muda mrefu,” Dkt Sing’oei alisema.
Kenya na Haiti zina uhusiano wa muda mrefu. Uhusiano huu ulirasimishwa mnamo Septemba 2023 na kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia.
Ushirikiano kati ya Kenya na Haiti
Msingi wa ushirikiano huu ni ushiriki wa Kenya katika ujumbe wa Mkakati Jumuishi wa Kiusalama nchini Haiti, ikisisitiza kujitolea kwake kuleta amani ya kimataifa na utulivu.
“Afrika na Haiti zina uhusiano wa kina wa kihistoria na kitamaduni. Ni wajibu wetu kuheshimu na kuimarisha uhusiano huu. Ustahimilivu na ujasiri wa Haiti unaendelea kututia moyo, na ni urithi huu wa pamoja ambao unatuchochea kujitolea kuisaidia Haiti katika changamoto zake za sasa.”
Kenya itaandaa tamasha ya Utamaduni ya Harmony4Haiti itakayofanyika Agosti 24, 2024.
Dkt Sing’oei alitangaza kuwa hafla hiyo, itakayoandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora na A4H, inalenga kuvumisha utamaduni wa Haiti kwa ulimwengu.